Thursday, August 13, 2015

MGEJA, GUNINITA RASMI CHADEMA



MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja amesema chama hicho kimeacha misingi yake na sasa kimegeuka kuwa ya kampuni.
Mbali na hilo, pia alimpiga kijembe mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli akimfananisha na dereva ambaye hajaweza kuendesha gari vizuri ‘learner’ akimaanisha kuwa hana uwezo wa kukiongoza chama hicho.
Mgeja alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akitangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku akiambatana na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita ambaye na yeye amejiunga na chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM, alisema ametumika ndani ya chama hicho kwa muda mrefu huku akishiriki kurekebisha kasoro mbalimbali zilizojitokeza lakini sasa imefika mwisho.
“Pamoja na kuzirekebisha kasoro zilizojitokeza mara kadhaa lakini kila jambo lina mwisho wake na kurekebisha mambo hayo nayo inafika mwisho.
“Chama sasa kimekuwa cha BMW yaani cha baba, mama na watoto. Kwa maana hiyo chama kimekuwa cha kampuni au familia ndio maana maoni ya wanachama na wananchi yanapuuzwa,”alisema.
Mgeja ambaye pia aliongozana na makada wengine wa chama hicho, alisema yeye pamoja na wenyeviti takribani 23, wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) pamoja na baadhi ya wabunge waliona mabadiliko yanahitajika ndani ya CCM.
“Matatizo ndani ya chama ni makubwa tunastahili tupate dereva fundi kwa sababu sisi tuliokitumikia chama tunakifahamu hapa tulipofika hivyo kinahitaji ukarabati mkubwa na tukashawishika kuwa Lowassa anaweza.
“Lakini kwa bahati mbaya mawazo ya wanachama, wananchi mwenyekiti wetu ameyapuuza. Nilikuwa navuta subira angekuwa muungwana angezungumza na kuomba radhi kwa aliyoyafanya kwani hayavulimiliki. Anakuja kwenye vikao vizito na akiwa na majina matano mfukoni.
 “Tukamwuliza atusomee sifa za hao wagombea watano lakini akafanya ubabe, akatengeneza nguvu kubwa, polisi wakazunguka lile jengo wakiwa na mabomu, farasi, gari ya maji ya washasha na hata ndani ya ukumbi polisi walikwepo wakiwa na mabomu.
“Nilimwuliza mwenyekiti kwamba leo tuko Burundi…tunawalalamikia kina Nkurunziza kumbe tunao wengi Tanzania. Tulipekuliwa na vijana wadogo wanakutana na hirizi zetu.
“Taswira ya chama imeondoka. Mliona kina Emmanuel Nchimbi walitoka wale hawakuwa wajinga waliona kasoro kubwa imefanyika,”alisema.
Alisema chama kimekuwa si kile cha wakati wa Mwalimu Nyerere kimejaa chuki, rushwa, fitna, kimepoteza mwelekeo na kwamba nguvu zilizotumika wakati wa kumpata mgombea urais ilikuwa hatari sana.
“Chama kilikuwa kinahitaji dereva fundi, lakini sasa kimekabidhiwa kwa Magufuli ambaye ni dereva leaner, hajawahi hata kuwa balozi wa nyumba kumi hata mimi hanifikii nusu, nilitegemea mwenyekiti wa chama angewaomba radhi wanachama lakini ameshindwa.
 “Mwenyekiti anakiacha chama vipande anaachaje kumweka Mwandosya kweli anazidiwa sifa na January Makamba, hata waziri mkuu wake ameshindwa kumwamini huku jana yake akimpongeza kuwa ni jembe lake.
 “Hata Sitta wakati ule wa spika alijitahidi ajibadilishe ikashindikana, sasa amemtumia bunge la katiba naye kachinjiwa mbali, Tyson, Sumaye wote wamechinjiwa mbali halafu anamuweka naibu waziri,”alisema.
Alisema kutokana na hayo ameamua kujiunga na Chadema kwenda kuongeza mapambano.
 “Kwanza nimuenzi Mwalimu Julius Nyerere aliposema kwamba watu wakiyataka mabadiliko wakayakosa ndani ya CCM wayatafute nje ya chama hiki. Sasa mimi ninamuenzi kwa moyo mkunjufu, nimeamua kuchana na CCM.
“Kwa heshima kabisa bila kumung’unya maneno natamka kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) tukapambane huko,”alisema Mgeja huku akikunja ngumi na kusema ‘peoples’.
Pia aliwataka makada wa chama chake ambao wamekuwa na tabia ya kurusha vijembe na kumchafua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wakapambane kwenye midahalo kwa hoja.
“Kama wao ni wanaume sasa twende kwenye midahalo wasimung’unye maneno kusema ukweli. Na haya niliyoyafanya mimi na wenzangu ndiyo maamuzi magumu,”alisema.
GUNINITA                                       
Kwa upande wake aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita alisema amezaliwa akiwa CCM na kwamba alikitumikia chama hicho kwa muda wa miaka 35, lakini kutokana na kukiukwa kwa misingi ameamua kuhama.
Alisema ni dhahiri kuwa vijana wadogo ambao wanawatukana viongozi wenye umri zaidi ya baba zao, wametumwa chama.
“Haiwezekani kijana mdogo anamtukana viongozi wakubwa huku chama kikikaa kimya na mwishoni kupata uongozi kwa utaratibu wa uyoga uyoga, sijui laana hii wataipeleka wapi,”alihoji Guninita.
Alisema CCM kilipofikia sasa kinakufa kama ilivyokuwa kwa chama cha KANU cha Kenya na UNIP ya nchini Zambia.
“Binadamu anapozaliwa anakuwa na malengo yake, inafika unaugua na kufa na sasa CCM kinaugua na majibu ya dokta ni lazima yaonyeshe kuwa kimekufa,”alisema.
Alisema makada wa chama hicho ambao wamekuwa wakimshambulia Lowassa watashughulikanao kwenye kampeni na kwamba waziri mkuu huyo zamani akae kimya kwa kuwa yeye anawamudu.
“Edward atuachie sisi tuna uwezo wa kuwamudu hawa makuruta wa siasa wa aina ya Nape,”alisema Guninita.
Mwisho.