WIZARA ya Elimu kwa kushirikiana na wadau wataendelea
kusimamia sera inayotaka kuondoa vikwazo vyote vinavyomsababisha mwanafunzi
kutohudhuria masomo.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Hedhi duniani leo
jijini Dar es Salaam, Afisa Elimu Mkuu wa Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi,
Madina Kemilembe alisema kukosekana kwa miundombinu rafiki mashuleni
kunasababisha wanafunzi kukosa masomo.
Alisema ukosefu wa mazingira bora kama vyoo, maji safi na
salama, sabuni ya kunawia pamoja chumba cha kubadilishia nguo hasa kwa watoto
wakike wanapokuwa hedhi mashuleni kunasababisha utoro mashuleni.
“Nawashukuru wadau Water Aid, Shirika la maendeleo la
Uholanzi(SNV), Kasole Secret pamoja na wengine kwa kuisaidia serikali kuandaa
mazingira rafiki kwa watoto wetu kwa kuwajengea vyumba vya kubadilishia na
kuwapelekea maji safi na upatikanaji wa pedi kwa baadhi ya shule,” alisema
Kemilembe.
Alisema kutokana na ukosefu wa pedi baadhi ya wanafunzi
wamekuwa wakitumia vitambaa visivyosalama na wanapovifua vinaanikwa chini ya
godoro hivyo kusababisha magonjwa mbalimbali kama fangasi kwa kutokauka vizuri.
Alisema ifikie wakati jamii ivunje ukimya kwa kuongelea
suala la hedhi kwa uwazi kwani linamyima mtoto wa kike masomo hasa kipindi
anapokuwa hedhi.
“Elimu itolewe kwa wazazi pamoja na wanafunzi wote wa kike
na wa kiume ili kuondoa unyanyapaa ili kuboresha mazingira ya kusoma kwa mtoto
wa kike,” alisema Kemilembe.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Girls in control
menstral hygien management kutoka Shirika la Maendeleo Uholanzi, Rozalia Mushi
alisema mradi wake utaendelea kuangalia jinsi ya kumsaidia mtoto wa kike
aliyeko mashuleni ili kumuongeza ufaulu katika masomo yake.
“Mtoto wa kike anakosa vipindi 450 kwa mwaka anapokuwa
katika hedhi kitu ambacho kinampunguzia ufaulu katika masomo yake kutokana na
kutokujiamini na unyanyapaa anapokuwa darasani,” alisema Mushi.
Alisema walimu pia walikuwa wakitoroka kufundisha kutokana
na kuwa katika hali hiyo hivyo waliamua kujenga vyumba vya kubadilishia katika
shule mbalimbali.
Nae Mkurugenzi wa Water Aid, Ibrahimu Kabole alisema kuna
uelewa mdogo pamoja na mila potofu zinazofanya jambo la hedhi kuonekana ni la
aibu.
“Asilimia 40 ya wanafunzi wa kike hutoroka shule kutokana
na kuzomewa,kunyanyapaliwa pamoja na kukosa mazingira rafiki wanapokuwa kwenye
hedhi,” alisema Kabole.
Alisema jamii ipewe uwezo kujua jambo hilo na liongelewe
kwa uwazi ili kuwajengea mazingira bora ya kusoma.
Siku ya hedhi duniani kwa
mara ya kwanza imeadhimishwa nchini kwa maandamano ya wanafunzi wa kike kutokea
Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi na kumalizikia viwanja vya mnazi mmoja
jijini Dar es Salaam.