Tuesday, November 10, 2015

NANI KUTWISHWA ZIGO LA KUFUFUA KILIMO NCHINI NA DK. MAGUFULI?



SEKTA ya kilimo ni moja ya sekta muhimu hapa nchini ambayo hapo zamani tuliita kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wetu.
Mara baada ya nchi yetu kupata Uhuru, Serikali ilitoa kipaumbele cha kwanza katika kuendeleza kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi wa nchi.
 Kilimo kiliajiri zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wote kwa mazao ya katani, kahawa na pamba yaliongoza kulipatia Taifa fedha za kigeni taifa hili.
kwa sasa ajira inayotokana na kilimo imeshuka hadi asilimia 80 tu ya watanzania ambapo pato la fedha za kigeni kutokana na mazao ya kibiashara limeshuka kutokana na kukosekana mipango na utekelezaji wa sera zinazosimamia sekta hii.

Katika awamu ya kwanza kumekuwapo kaulimbiu na maazimio mbalimbali kama vile “Chakula ni Uhai”, “Siasa ni Kilimo”,“Kilimo cha Kufa na Kupona”, “Mvua za Kwanza ni za Kupandia” ili kuhamasisha maendeleo ya kilimo, pamoja na kuhamasisha kilimo cha ujamaa.
Awamu ya Pili iliongozwa na Rais Ali Hassan Mwinyi ambapo tulishuhudia mageuzi ya kiuchumi ambayo yalikuwa kichocheo kikubwa katika maendeleo ya kilimo ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Sera ya Kilimo ya mwaka 1983.
Awamu ya tatu ya uongozi ilikuwa chini ya Rais Benjamin William Mkapa ambapo katika awamu hiyo kilimo kilipata msukumo wa kipekee kwa kuonyesha mwelekeo Katika awamu hiyo kutokana na
utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kilimo na Mifugo ya mwaka 1997 na uanzishwaji wa Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo ulishuhudia kilimo kikikua kutoka chini ya asilimia 3 hadi asilimia 6 kulinganisha na awamu zilizotangulia.

Awamu ya nne ya uongozi ambayo ipo chini ya Rais Dk. Jakaya Kikwete, licha ya kilimo kuendelea kupewa kipaumbele kikubwa, kwa kaulimbiu mbadala ya kilimo kwanza pamoja na utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) na Programu ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika (CRMP) ambazo zimekuwa chachu ya kuleta mapinduzi ya kijani hapa nchini lakini lengo halikutimia ipasavyo kutokana na

Licha ya hayo Jambo kubwa la kujivunia kutokana na kilimo ni kuwa
kwa sasa asilimia 95 ya mahitaji ya Taifa ya chakula kinazalishwa hapa hapa nchini kwa Serikali kuweka mfumo wa kuhifadhi chakula kwa ajili ya matumizi wakati upungufu unapotokea ili kukabiliana na baa la njaa. Takwimu zinadhihirisha kwamba akiba ya Taifa ya Chakula imekuwa ikiongezeka kila mwaka na uwezo wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unatarajia kufikia tani 400,000.

Kwa takribani miongo mitano na ushei ya Uhuru wa nchi yetu, pamoja na kuwa na changamoto nyingi za kisiasa, kijamii na kiuchumi, kilimo chetu kimeendelea kuwa nguzo kuu na mhimili wa kujitoshereza kwa chakula tu.
Lakini iwapo tutakuwa na uthubutu wa kuwekeza inavyopaswa katika kilimo tutaweza si tu kujitoshereza kwa chakula bali pia kupiga hatua za maendeleo kwa sekta hiyo adhimu, pengine kiasi cha kurudisha tija kubwa ya pato la kigeni inayoweza kupatikana kwa kurekebisha mikakati ya mazao ya kibiashara kwa kulenga mahitaji ya sasa ya soko.

Kimsingi baadhi ya maeneo muhimu yanayopaswa kuangaziwa na awamu ya tano ya serikali ili kukirudishia kilimo hadhi yake kamili ni pamoja na tathmini muafaka ya kilichosababisha kudorora kwa sekta hiyo, ili kubaini nini kifanyike kiutekelezaji ili kufikia ufanisi wa hali ya juu.
Mathalan, baadhi ya maeneo muhimu yanayopaswa kutazamwa upya ni pamoja na upatikanaji nafuu wa pembejeo ambao umekuwa ukisuasua kutokana na gharama kuwa kubwa ukilinganisha na uwezo wa wakulima wetu.
Uwekezaji muafaka wa mbinu za kisasa za kilimo kwa kuzingatia matumizi ya nyenzo, mbolea, kubaini aina ya mazao yanayofaa kulimwa katika ardhi husika pamoja na kuboresha weledi wa maafisa ughani katika kusimamia kiklimo cha kimapinduzi, kitakacholitoa taifa letu katyika kilimo cha mazoea kwa ajili ya chakula lakini kikakidhi pia mahitaji ya kibiashara na kiuchumi.

Kwa historia ya sekta hiyo hapa nchini kuna mengi tunayoweza kutohoa kutokana na utekelezaji wa miaka iliyopita, mojawapo ni kuwepo kwa mashamba ya ushirikika kwa kuwa kimsingi licha ya mengi kati ya mashamba hayo kufa kifo cha asili lakini bado vyama vya ushirikika vipo. Ni suala la kugeuza tu mashamba yaliyokuwa katyika muundo huo hata yaliyomilikiwa na serikali, kuwa mikononi mwa wakulima lakini msisitizo ukiwekwa katika upatikanaji masoko ya kuuzia mazao yatakayovunwa.

Hayo yakitekelezwa vyema dhima nzima ya uwepo wa viwanda ili vitumie ghafi muhimu inayozalishwa kwa kilimo, ndipo itaweza kutimia kikamilifu kwa kuwa soko la dunia la kilimo kwa sasa limeegemea bidhaa zitokanazo na kilimo zilizokuwa tayari kwa matumizi na si ghafi inayopaswa kuandaliwa kuwa bidhaa.
hiyo mikakati ya serikali ya awamu ya tano iliyojinasibu kufufua viwanda wakati wa kampeni itatimia si kwa kuangalia upande huo tu, bila kuhusisha kilimo kwa kuwa ilidhihirika wazi wakati wa awamu ya kwanza zao la pamba lilikuwa na soko kubwa la ndani kutokana na kuwepo viwanda vingi vya kuzalisha nguo, kabla ya ziada kuuzwa nje na kutupatia fedha za kigeni.

Kuwekeza kwenye viwanda sanjari na kilimo kuna faida nyingi kwa kuwa tumezungukwa na masoko yaliyo tayari kupokea bidhaa zetu katika jumuiya zinazotuzunguka ikiwemo SADC na EAC anvayo kwa sasa ina soko kubwa zaidi kwa kuwa inajumuisha nchi tano, tofauti na ilivyokuwa awali ilipoundwa na nchi tatu.
Tukienda mbali zaidi kuna fursa za kimataifa kama ule mpango wa AGOA ambao bado unatuwezwesha kupata pato kubwa la kigeni nchini Marekani, bila gharama ya tozo la ushuru wa kuingiza bidhaa nchini humo.

Na kwa kuwa kinara wa awamu ya rtanio Raisi Magufuli anatokea katika wizara ya ujenzi na awali alitumikia uchukuzi na uvuzi, tunaamini akiunganisha vyote hivyo na kunasibisha kilimo naviwanda uchumi utakuwa kwani bidhaa zinazozalishwa zinahitaji miundo mbinu bora kufikia walaji wa ndani na nchi jirani…

Lakini ili kufikia mafanikio ya kiwango cha juu kwa sekta hizo zinazotegemeana kuna haja ya makusudi ya kutathmini baadhi ya changamoto zilizosababisha kilimo kidumae zikiwemo ardhi ya kilimo kutotambulika kisheria hivyo kubadilishwa matumizi, jambo linalozalisha migogoro holela baina ya wawekezaji na wananchi wazawa waliomilikishwa maeneo kwa njia ya kurithi.
Mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha kilimo kushindwa kutoa ajira kutokana na upungufu wa mvua, jangwa na kuongezeka kwa joto duniani.

 Ushiriki hafifu wa sekta binafsi katika kilimo ambapo sekta nyingi zimejikita kuwekeza katika fani nyingine.

 Ushiriki hafifu wa vijana katika kilimo ambao ndio mguvu kazi na rasilimali watu kwa kuwa ndio wenye nguvu na uwezo mkubwa, kukikwepa kilimo kwa kukimbilia mijini kufanya biashara zisizo endelevi.
              
Uwezo mdogo wa wakulima kununua zana bora na pembejeo za kilimo
 Miundombinu duni katika maeneo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo

Msukumo wa kuzalisha mazao ya nishati mbadala na madhara yake unakinzana na lengo kuu la kuzalisha mazao ya chakula kwa baadhi ya wakulima ambapo wengi huangazia kilimo cha chakula na kuachana na mazao ya biashara.

Gharama kubwa ya ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na maghara ya kuhifadhia mazao pindi yanapovunwa.

Uvamizi wa visumbufu vya mimea yanayoshindikana kudhibitiwa ambavyo ni pamoja na wadudu na magonjwa mbalim bali ya mimea.

Elimu duni walionayo wakulima pamoja na wadau wa mbalimbali wa kilimo juu ya masuala ya ushirika pamoja na vyama hivi kukosa mitaji na kubaki vikikopa mazao ya wakulima.
Usimamizi hafifu wa sera ya soko huru ambapo dhana hiyo imekuwa kinyume na matarajio ya wengi na sasa ni kama soko holela lisilokuwa na mdhibiti.
Idadi ndogo ya wataalam wa kilimo na ushirika pamoja na maslahi duni ukilinganisha na mazingira wanakohitajika kufanya kazi.
Kukosekana kwa mikopo yenye masharti nafuu ya kuendeleza kilimo kwa mabenki mengi kukwepa kukopesha sekta hiyo kwa kuichukulia kuwa Nyanja isiyotabirika katika uwezo wa kurudisha mikopo.

Kimsingi pia lazima kuwekeza kwa vivutio vya makusudi vitakavyosababisha nguvu kazi kubwa hususan vijana kujishugulisha na kilimo kama njia ya kuendesha maisha yao na kubadili mtazamo mzima juu ya sekta hiyo, kwa kurejesha hamasa za kimatendo zaidi kwa kutumia mbinu za zamani kwa mabadiliko ya kisasa kuanzia ngazi za awali kabisa za mafunzo ya vinaja wetu katika ngazi mbalimbali za elimu ili wasikikimbie kilimo badala yake wavutiwe nacho. 
Kwa kutimiza hayo na mengine muambatano naamini kauli mbiu ya HAPA KAZI TU itajisadikisha ipasavyo kwenye sekta ya kilimo maana matokeo ya kazi ni tija stahiki.
0762656400 KWA MAWASILIANO 

Wednesday, October 14, 2015

MTIKISIKO UCHUMI SUPERMARKET



HALI yasintofahamu katika kampuni ya Uchumi ya jijini Dar es Salaam inayomilikiwa na wakenya jana ilisababisha kazi kusimama kwa siku nzima baada ya wafanyakazi wake kuutaka uongozi kuwaeleza hatima ya ajira na mafao yao baada ya kampuni hiyo kuonekana kuyumba.
Kutokana na sintofahamu hiyo wafanyakazi na waajiri wa kampuni hiyo juzi walilazimika kulala ofisini baada ya wafanyakazi hao kuwazuia kutokana hadi wapate majibu ya hatima yao.
Waandishi waliwashuhudia wafanyakazi hao na waajiri wakiwa ndani na milango ikiwa imefungwa hakuna anayetoka wala kuingia huku wafanyakazi waliolala nje wakiwapitishia vyakula wenzao chini ya milango pamoja na kuwapa maji yakiwa kwenye chupa zilizowekewa mirija ambayo ilikuwa ikipitishwa sehemu ambazo zilikuwa na uwazi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mlango kufunguliwa na kuruhusiwa kutoka nje,
Mjumbewa Chama cha Wafanyakazi ambaye pia ni mfanyakazi wa kampuni ya Uchumi, GeofreyMuyenzi, 
alisema kuwa kutokana na kuyumba kwa kampuni hiyo waliwaandikia barua waajiri wao ya kuwataka kuwaeleza hatima yao lakini hawakupatiwa majibu.
Alisema kutokana na madeni iliyonayo kampuni hiyo wamelazimika kuulizia hatima yao na kwamba mpaka leo (jana) hatujapatiwa majibu na badala yake baada ya kikao kilichofanyika dhidi ya Chama cha Wafanyakazi. 
Wizara ya Kazi pamoja na waajiri na wanasheria wa kampuni wameahidi kutoa majibu keshokutwa.
“Madeni katika kampuni hii yamezidi na wasambazaji hawaleti tena mizigo yao huku wengine wameanza kuiondoa pia deni la pango limekuwa kubwa kiasi kwamba tunahisi anaweza kuja kufungia mali zawatu wakati wowote,” alisemaMuyenzi.
Naye Katibu wa Chama cha WafanyakaziWilaya yaTemeke (TUICO), George Namkinga alisema kuwa wamekaa katika kikao na uongozi pamoja na wafanyakazi na kukubaliana kuwa majibu yatapatikana kutoka Nairobi keshokutwa katika kingine kikao kitakachowahusishaTUICO mkoa, Serikali, wanasheria wa kampuni pamoja na wafanyakazi lengo ni ili wafanyakazi wapate kujua hatima yao.
Alisema pia lengo ni kampuni iweze kuendelea ili wafanyakazi waweze kuendelea na kazi lakini iwapo ikishindwa kuendelea ndipo sheria zitachukuliwa ili kuwawezesha kupata hatima yao.
“Kweli kampuni ilisuasua na mishahara ikawa inasuasua pia lakini tumefikia pazuri kutokana na kuwa uongozi umejikomiti kwamba kuna jibu na kule Nairobi wametuma wanasheria na tumeweka makubaliano kisheria hivyo hakuna kitakachoharibika,” alisema Namkinga.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kampuni hiyo ambazo BLOG HII ilizipata, inadaiwa zaidi ya bilioni nne kutoka kwa watu mbalimbali.
BLO HII  ilimtafuta Meneja wa kampuni hiyo nchini kwa njia ya simu Benard Muthin, kuzungumzia madai hayo alisema kuwa hana mamlaka ya kuzungumzia madai hayo.
“Mimi sina mamlaka ya kuzungumzia madai hayo labda niwatumie namba ya simu ya ofisini ili muwatafute wazungumzaji wanaoweza kuzungumzia madai hayo.

Thursday, August 13, 2015

MGEJA, GUNINITA RASMI CHADEMA



MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja amesema chama hicho kimeacha misingi yake na sasa kimegeuka kuwa ya kampuni.
Mbali na hilo, pia alimpiga kijembe mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli akimfananisha na dereva ambaye hajaweza kuendesha gari vizuri ‘learner’ akimaanisha kuwa hana uwezo wa kukiongoza chama hicho.
Mgeja alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akitangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku akiambatana na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita ambaye na yeye amejiunga na chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM, alisema ametumika ndani ya chama hicho kwa muda mrefu huku akishiriki kurekebisha kasoro mbalimbali zilizojitokeza lakini sasa imefika mwisho.
“Pamoja na kuzirekebisha kasoro zilizojitokeza mara kadhaa lakini kila jambo lina mwisho wake na kurekebisha mambo hayo nayo inafika mwisho.
“Chama sasa kimekuwa cha BMW yaani cha baba, mama na watoto. Kwa maana hiyo chama kimekuwa cha kampuni au familia ndio maana maoni ya wanachama na wananchi yanapuuzwa,”alisema.
Mgeja ambaye pia aliongozana na makada wengine wa chama hicho, alisema yeye pamoja na wenyeviti takribani 23, wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) pamoja na baadhi ya wabunge waliona mabadiliko yanahitajika ndani ya CCM.
“Matatizo ndani ya chama ni makubwa tunastahili tupate dereva fundi kwa sababu sisi tuliokitumikia chama tunakifahamu hapa tulipofika hivyo kinahitaji ukarabati mkubwa na tukashawishika kuwa Lowassa anaweza.
“Lakini kwa bahati mbaya mawazo ya wanachama, wananchi mwenyekiti wetu ameyapuuza. Nilikuwa navuta subira angekuwa muungwana angezungumza na kuomba radhi kwa aliyoyafanya kwani hayavulimiliki. Anakuja kwenye vikao vizito na akiwa na majina matano mfukoni.
 “Tukamwuliza atusomee sifa za hao wagombea watano lakini akafanya ubabe, akatengeneza nguvu kubwa, polisi wakazunguka lile jengo wakiwa na mabomu, farasi, gari ya maji ya washasha na hata ndani ya ukumbi polisi walikwepo wakiwa na mabomu.
“Nilimwuliza mwenyekiti kwamba leo tuko Burundi…tunawalalamikia kina Nkurunziza kumbe tunao wengi Tanzania. Tulipekuliwa na vijana wadogo wanakutana na hirizi zetu.
“Taswira ya chama imeondoka. Mliona kina Emmanuel Nchimbi walitoka wale hawakuwa wajinga waliona kasoro kubwa imefanyika,”alisema.
Alisema chama kimekuwa si kile cha wakati wa Mwalimu Nyerere kimejaa chuki, rushwa, fitna, kimepoteza mwelekeo na kwamba nguvu zilizotumika wakati wa kumpata mgombea urais ilikuwa hatari sana.
“Chama kilikuwa kinahitaji dereva fundi, lakini sasa kimekabidhiwa kwa Magufuli ambaye ni dereva leaner, hajawahi hata kuwa balozi wa nyumba kumi hata mimi hanifikii nusu, nilitegemea mwenyekiti wa chama angewaomba radhi wanachama lakini ameshindwa.
 “Mwenyekiti anakiacha chama vipande anaachaje kumweka Mwandosya kweli anazidiwa sifa na January Makamba, hata waziri mkuu wake ameshindwa kumwamini huku jana yake akimpongeza kuwa ni jembe lake.
 “Hata Sitta wakati ule wa spika alijitahidi ajibadilishe ikashindikana, sasa amemtumia bunge la katiba naye kachinjiwa mbali, Tyson, Sumaye wote wamechinjiwa mbali halafu anamuweka naibu waziri,”alisema.
Alisema kutokana na hayo ameamua kujiunga na Chadema kwenda kuongeza mapambano.
 “Kwanza nimuenzi Mwalimu Julius Nyerere aliposema kwamba watu wakiyataka mabadiliko wakayakosa ndani ya CCM wayatafute nje ya chama hiki. Sasa mimi ninamuenzi kwa moyo mkunjufu, nimeamua kuchana na CCM.
“Kwa heshima kabisa bila kumung’unya maneno natamka kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) tukapambane huko,”alisema Mgeja huku akikunja ngumi na kusema ‘peoples’.
Pia aliwataka makada wa chama chake ambao wamekuwa na tabia ya kurusha vijembe na kumchafua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wakapambane kwenye midahalo kwa hoja.
“Kama wao ni wanaume sasa twende kwenye midahalo wasimung’unye maneno kusema ukweli. Na haya niliyoyafanya mimi na wenzangu ndiyo maamuzi magumu,”alisema.
GUNINITA                                       
Kwa upande wake aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita alisema amezaliwa akiwa CCM na kwamba alikitumikia chama hicho kwa muda wa miaka 35, lakini kutokana na kukiukwa kwa misingi ameamua kuhama.
Alisema ni dhahiri kuwa vijana wadogo ambao wanawatukana viongozi wenye umri zaidi ya baba zao, wametumwa chama.
“Haiwezekani kijana mdogo anamtukana viongozi wakubwa huku chama kikikaa kimya na mwishoni kupata uongozi kwa utaratibu wa uyoga uyoga, sijui laana hii wataipeleka wapi,”alihoji Guninita.
Alisema CCM kilipofikia sasa kinakufa kama ilivyokuwa kwa chama cha KANU cha Kenya na UNIP ya nchini Zambia.
“Binadamu anapozaliwa anakuwa na malengo yake, inafika unaugua na kufa na sasa CCM kinaugua na majibu ya dokta ni lazima yaonyeshe kuwa kimekufa,”alisema.
Alisema makada wa chama hicho ambao wamekuwa wakimshambulia Lowassa watashughulikanao kwenye kampeni na kwamba waziri mkuu huyo zamani akae kimya kwa kuwa yeye anawamudu.
“Edward atuachie sisi tuna uwezo wa kuwamudu hawa makuruta wa siasa wa aina ya Nape,”alisema Guninita.
Mwisho.

Monday, July 6, 2015

TTCL KUPELEKA MAWASILIANO KWA WATEJA WALIO NJE YA MKONGO



KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL), imeanza kuwawezesha wateja wake yakiwamo makampuni, taasisi na ofisi za Serikali kupata mawasiliano ya intaneti sehemu zilizo mbali na njia ya mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Taarifa hiyo ilitolewa na Ofisa Mtatuzi wa Masuala ya Kiufundi wa TTCL, Fredrick Bernad alipokuwa akizungumza katika Maonesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam maarufu kama maonyesho ya Sabasaba.
Kwa mujibu wa Benard, teknolojia hiyo ni mpya na ni muhimu kwa kampuni na wateja wengine kwani ni bora na ni ya uhakika kwa mawasiliano.
“Mbali na mawasiliano ya intaneti, wateja wanaweza pia kupata huduma ya kupata mawasiliano ya shughuli za kiofisi zaidi ya mbili ambazo zipo maeneo tofauti na kushirikiana kwa taarifa na mifumo ya kompyuta iitwayo Mpls Vpn.

“TTCL iliamua kuleta huduma hiyo kutokana na mahitaji makubwa ya matumizi ya intaneti kwa shughuli za maendeleo kwani kuna maeneo ambayo awali yalihitaji huduma ya mkongo lakini kutokana na umbali pamoja na gharama imekuwa ngumu kuwapelekea huduma.