Monday, January 4, 2016

MUHIMBILI YAFUNGA CT SCAN MPYA



SERIKALI imefunga mashine mpya ya CT Scan yenye gharama ya sh.  Milioni 1.7 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH yenye uwezo wa kupiga picha zaidi ya 128 ikilinganishwa na ya awali iliyokuwa ikipiga picha sita.
Hatua hiyo imekuja kutokana na mashine iliyokuwa imefungwa awali kuharibika kila mara na kusababisha usumbufu makubwa kwa wagonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana hospitalini hapo wakati wa ziara ya kushtukiza, Naibu waziri wa wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, dk. Hamis kigwangwala alisema hiyo ni hatua nzuri kwa serikali ya awamu ya tano na kwamba wamejipanga kufanya mambo makubwa.
"Nashukuru kwamba maagizo yaliyotolewa yametekelezwa katika kipindi kifupi, hii inadhihirisha kwamba tukishirikana kwa namna hii tutatoa huduma bora kwa watanzania, tumeanza hapa Muhimbili tutakwenda na hospitali zetu za Dodoma na Mwanza, " alisema
Dk kigwangwala alitaka Kaimu Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru na watendaji wengine kuboresha utoaji wa huduma ili kuwavutia watendaji wake.
 
“Ni lazima tuboreshe huduma ili kuwavutia hata wale wanaokwenda kuhudumiwa katika vituo vya watu binafsi lakini pia naiagiza Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kuondoa MNH katika kundi la pamoja na hospitali nyingine kuanzia sasa kwani haina hadhi sawa na zingine. Hapa tunatoa huduma si kutaka fedha za wagonjwa "alisema.

Kwa upande wake Profesa Museru alisema tayari wamekamilisha Ujenzi wa jengo jipya la icu pamoja na kutengeneza mfumo wa matibabu bila ya kubeba makaratasi (Paperless).
 
"Taarifa za mgonjwa zinahamishwa kwa kutumia mfumo wa komputa tumeanza katika kitengo cha wagonjwa wa dharura (emergence) na tunatarajia hivi karibuni kuweka  komputa 48 wodini ili kuwawezesha madaktari wa vitengo vingine waweze kupokea mafaili hayo,” alisema.

Awali Dk. Kigwangwala alianza ziara yake hiyo ya kushtukiza kwenye ofisi za kitengo cha Mpango wa Damu Salama zilizoko ilala jijini hapa.
Alisema hiyo ilitokana na malalamiko mengi aliyoyapokea wakati alipokuwa katika ziara zake mikoa mbalimbali kuhusu upungufu wa damu nchini hasa katika hospitali za Pembezoni.
Aliziagiza Halmashauri zote kuhakikisha zinatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya bajeti ya kuwezesha ukusanyaji wa damu salama.
Aidha aliutaka mfuko wa NHIF kuanza kuitenga fedha kwa ajili   ya kuchangia mifuko inayotumiwa kuhifadhia damu.
“Hatuuzi damu lakini tunataka mfuko huu uanze kuchangia angalau mifuko ya kuhifadhia damu inayopatikana hatuwezi kutoa kila kitu bure, ni lazima tuanze kusaidia kitengo hiki kukusanya damu kwa wakati,” alisema

WASICHANA WATATU KUJENGEWA UWEZO



WASICHANA watatu kati ya 26 wamechaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika mafunzo ya kuwajengea uwezo yanayoshirikisha mataifa mbalimbali duniani.
Mafunzo hayo yanayotolewa kupitia programu ya kubadilishana mabinti walioko katika vyama vya skauti wanawake duniani, yanashirikisha nchi za Tanzania, Rwanda, Afrika Kusini, Madagascar na Kenya.
Wasichana hao na nchi wanazokwenda ni Rose Mwambeta (Rwanda), Happines Mshana (Madagascar) na Mwaka Rashidi (Afrika Kusini).
Akizungumza jana wakati wa kuwakabidhi bendera na kuwaaga wasichana hao, Kamishna wa Tanzania Girl Guide, Symphrosa Hangi, alisema wasichana hao watakaa katika nchi hizo kwa miezi sita huku wakijifunza mambo mbalimbali.
“Nasisi pia tutawapokea wasichana watatu kutoka nchi hizo ambao watakaa hapa kwetu kwa miezi sita, kupitia kwao tutajifunza waliyokuwa wanayafanya na wao watajifunza mambo tunayoyafanya sisi,” alisema Hangi.
Alisema mchakato wa kuwapata wasichana hao ulitangazwa kwenye vyombo vya habari ambapo walijitokeza 26 na kuchujwa kisha wakapatikana watatu waliokidhi vigezo. Vigezo ni kuwa na umri kati ya miaka 18-25 na elimu ya kiwango cha stashahada.
Naye Mratibu wa Miradi wa Tanzania Girl Guide, Agnes Fivawo, alisema mambo watakayojifunza wasichana hao ni pamoja na utawala, ukufunzi na ujasiriamali.
“Tunabadilishana mabinti kutoka nchi moja kwenda nyingine ili waweze kujifunza mambo ya girl guide kwani yatawasaidia kukua kiakili, kujitegemea na hivyo kufanya mambo yao wenyewe,” alisema Fivawo.
Alisema wakiwa huko wasichana hao watapangiwa nyumba za kuishi na watakuwa wakilipwa posho ya kujikimu kila mwezi.