WASICHANA watatu kati ya 26 wamechaguliwa kuiwakilisha
Tanzania katika mafunzo ya kuwajengea uwezo yanayoshirikisha mataifa mbalimbali
duniani.
Mafunzo hayo yanayotolewa kupitia programu ya kubadilishana
mabinti walioko katika vyama vya skauti wanawake duniani, yanashirikisha nchi
za Tanzania, Rwanda, Afrika Kusini, Madagascar na Kenya.
Wasichana hao na nchi wanazokwenda ni Rose Mwambeta
(Rwanda), Happines Mshana (Madagascar) na Mwaka Rashidi (Afrika Kusini).
Akizungumza jana wakati wa kuwakabidhi bendera na kuwaaga
wasichana hao, Kamishna wa Tanzania Girl Guide, Symphrosa Hangi, alisema
wasichana hao watakaa katika nchi hizo kwa miezi sita huku wakijifunza mambo
mbalimbali.
“Nasisi pia tutawapokea wasichana watatu kutoka nchi hizo
ambao watakaa hapa kwetu kwa miezi sita, kupitia kwao tutajifunza waliyokuwa
wanayafanya na wao watajifunza mambo tunayoyafanya sisi,” alisema Hangi.
Alisema mchakato wa kuwapata wasichana hao ulitangazwa
kwenye vyombo vya habari ambapo walijitokeza 26 na kuchujwa kisha wakapatikana
watatu waliokidhi vigezo. Vigezo ni kuwa na umri kati ya miaka 18-25 na elimu
ya kiwango cha stashahada.
Naye Mratibu wa Miradi wa Tanzania Girl Guide, Agnes
Fivawo, alisema mambo watakayojifunza wasichana hao ni pamoja na utawala,
ukufunzi na ujasiriamali.
“Tunabadilishana mabinti kutoka nchi moja kwenda nyingine
ili waweze kujifunza mambo ya girl guide kwani yatawasaidia kukua kiakili,
kujitegemea na hivyo kufanya mambo yao wenyewe,” alisema Fivawo.
Alisema wakiwa huko wasichana hao watapangiwa nyumba za
kuishi na watakuwa wakilipwa posho ya kujikimu kila mwezi.
No comments:
Post a Comment