Monday, January 4, 2016

MUHIMBILI YAFUNGA CT SCAN MPYA



SERIKALI imefunga mashine mpya ya CT Scan yenye gharama ya sh.  Milioni 1.7 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH yenye uwezo wa kupiga picha zaidi ya 128 ikilinganishwa na ya awali iliyokuwa ikipiga picha sita.
Hatua hiyo imekuja kutokana na mashine iliyokuwa imefungwa awali kuharibika kila mara na kusababisha usumbufu makubwa kwa wagonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana hospitalini hapo wakati wa ziara ya kushtukiza, Naibu waziri wa wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, dk. Hamis kigwangwala alisema hiyo ni hatua nzuri kwa serikali ya awamu ya tano na kwamba wamejipanga kufanya mambo makubwa.
"Nashukuru kwamba maagizo yaliyotolewa yametekelezwa katika kipindi kifupi, hii inadhihirisha kwamba tukishirikana kwa namna hii tutatoa huduma bora kwa watanzania, tumeanza hapa Muhimbili tutakwenda na hospitali zetu za Dodoma na Mwanza, " alisema
Dk kigwangwala alitaka Kaimu Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru na watendaji wengine kuboresha utoaji wa huduma ili kuwavutia watendaji wake.
 
“Ni lazima tuboreshe huduma ili kuwavutia hata wale wanaokwenda kuhudumiwa katika vituo vya watu binafsi lakini pia naiagiza Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kuondoa MNH katika kundi la pamoja na hospitali nyingine kuanzia sasa kwani haina hadhi sawa na zingine. Hapa tunatoa huduma si kutaka fedha za wagonjwa "alisema.

Kwa upande wake Profesa Museru alisema tayari wamekamilisha Ujenzi wa jengo jipya la icu pamoja na kutengeneza mfumo wa matibabu bila ya kubeba makaratasi (Paperless).
 
"Taarifa za mgonjwa zinahamishwa kwa kutumia mfumo wa komputa tumeanza katika kitengo cha wagonjwa wa dharura (emergence) na tunatarajia hivi karibuni kuweka  komputa 48 wodini ili kuwawezesha madaktari wa vitengo vingine waweze kupokea mafaili hayo,” alisema.

Awali Dk. Kigwangwala alianza ziara yake hiyo ya kushtukiza kwenye ofisi za kitengo cha Mpango wa Damu Salama zilizoko ilala jijini hapa.
Alisema hiyo ilitokana na malalamiko mengi aliyoyapokea wakati alipokuwa katika ziara zake mikoa mbalimbali kuhusu upungufu wa damu nchini hasa katika hospitali za Pembezoni.
Aliziagiza Halmashauri zote kuhakikisha zinatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya bajeti ya kuwezesha ukusanyaji wa damu salama.
Aidha aliutaka mfuko wa NHIF kuanza kuitenga fedha kwa ajili   ya kuchangia mifuko inayotumiwa kuhifadhia damu.
“Hatuuzi damu lakini tunataka mfuko huu uanze kuchangia angalau mifuko ya kuhifadhia damu inayopatikana hatuwezi kutoa kila kitu bure, ni lazima tuanze kusaidia kitengo hiki kukusanya damu kwa wakati,” alisema

No comments:

Post a Comment