Sunday, May 24, 2015

VIJANA WASEMA RUFIJI KURA YA MAONI PATACHIMBIKA



VIJANA wa wilaya ya Rufiji wameamua kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi hasa kipindi cha kura za maoni ili kujenga uelewa kwa wananchi hao .
Wakizungumza jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti vijana hao walisema wameamua kutoa elimu hiyo ili kuubadilisha mfumo uliopo hasa ndani ya Chama cha Mapinduzi(Ccm) ambao unawanyima haki ya kuchagua kiongozi bora.
Mmoja kati ya vijana hao,Juma Kiholobele alisema mfumo uliopo unasababisha watu wenye fedha kuwa ndio wenye haki ya kuwa viongozi.
“Tunaenda kuwaeleza wenzetu wasiojua kabisa, wanaojua kidogo na wanaojua sana kuwa lazima mfumo urudi kama ulivyoasisiwa ambapo tulikuwa tukiangalia uwezo wa mtu katika uongozi,” alisema Kiholobele.
Alisema mfumo wa kugawa fedha kipindi cha uchaguzi unawanyima wananchi haki ya kusikiliza sera na malengo ya mgombea.
“Tutapambana na mfumo uliopo ambao fedha zinatumika kama raslimali ya kupata uongozi ambapo mamlaka yanabaki kwenye familia chache zenye kipato,” alisema Kiholobele.
Alisema mfumo huo unasababisha watu wenye fedha kuwa wizi kwa kuwa itabidi warudishe mitaji yao(fedha) waliyotoa kipindi cha uchaguzi hivyo kurudisha maendeleo ya nchi nyuma.
Alisema mabadiliko yapatikane ndani ya CCM ikishindikana watayatafuta nje.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Uvccm wilayani Rufiji, Shabani Matwebe alisema atahakikisha wanachama, viongozi na mashabiki wa CCM wanafuata katiba na kanuni za chama hicho katika kupata wagombea.
“Vijana tuone kama tumechelewa kuubadili mfumo huu kwani katiba na kanuni za CCM katika kupata wagombea tunazijua na ni lazima sasa tuzitumie na si kusubiri nani ana fedha nyingi mwaka huu,” alisema Matwebe.
Alisema kura za maoni mwaka huu ndani ya chama hicho zitakuwa za ushindani kama CHADEMA na CCM kutokana na watu kuelimika kupitia wao.
Nae mwanachama wa ccm, Jamvi Magawa alisema rushwa ndani ya CCM ndiyo chanzo cha tatizo la ukosefu wa maadili ndani ya chama hicho.
“Kwa sababu ya rushwa tumeendelea kuonewa na kunyanyaswa kwani hatuna mamlaka ya kumuuliza kiongozi ambae tulimchagua kwa wingi wa fedha zake kwa sababu tulikula 15,000 zake mwaka 2010,” alisema Magawa.
Alisema viongozi wanapokuwa vipofu kuona matatizo ya wananchi wao, wananchi watakuwa viziwi hawatawasikiliza viongozi wao.
                       





  
 

No comments:

Post a Comment