Thursday, May 28, 2015

HEDHI SALAMA KWA MWANAFUNZI IMESISITIZWA



WIZARA ya Elimu kwa kushirikiana na wadau wataendelea kusimamia sera inayotaka kuondoa vikwazo vyote vinavyomsababisha mwanafunzi kutohudhuria masomo.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Hedhi duniani leo jijini Dar es Salaam, Afisa Elimu Mkuu wa Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi, Madina Kemilembe alisema kukosekana kwa miundombinu rafiki mashuleni kunasababisha wanafunzi kukosa masomo.
Alisema ukosefu wa mazingira bora kama vyoo, maji safi na salama, sabuni ya kunawia pamoja chumba cha kubadilishia nguo hasa kwa watoto wakike wanapokuwa hedhi mashuleni kunasababisha utoro mashuleni.
“Nawashukuru wadau Water Aid, Shirika la maendeleo la Uholanzi(SNV), Kasole Secret pamoja na wengine kwa kuisaidia serikali kuandaa mazingira rafiki kwa watoto wetu kwa kuwajengea vyumba vya kubadilishia na kuwapelekea maji safi na upatikanaji wa pedi kwa baadhi ya shule,” alisema Kemilembe.
Alisema kutokana na ukosefu wa pedi baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakitumia vitambaa visivyosalama na wanapovifua vinaanikwa chini ya godoro hivyo kusababisha magonjwa mbalimbali kama fangasi kwa kutokauka vizuri.
Alisema ifikie wakati jamii ivunje ukimya kwa kuongelea suala la hedhi kwa uwazi kwani linamyima mtoto wa kike masomo hasa kipindi anapokuwa hedhi.
“Elimu itolewe kwa wazazi pamoja na wanafunzi wote wa kike na wa kiume ili kuondoa unyanyapaa ili kuboresha mazingira ya kusoma kwa mtoto wa kike,” alisema Kemilembe.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Girls in control menstral hygien management kutoka Shirika la Maendeleo Uholanzi, Rozalia Mushi alisema mradi wake utaendelea kuangalia jinsi ya kumsaidia mtoto wa kike aliyeko mashuleni ili kumuongeza ufaulu katika masomo yake.
“Mtoto wa kike anakosa vipindi 450 kwa mwaka anapokuwa katika hedhi kitu ambacho kinampunguzia ufaulu katika masomo yake kutokana na kutokujiamini na unyanyapaa anapokuwa darasani,” alisema Mushi.
Alisema walimu pia walikuwa wakitoroka kufundisha kutokana na kuwa katika hali hiyo hivyo waliamua kujenga vyumba vya kubadilishia katika shule mbalimbali.
Nae Mkurugenzi wa Water Aid, Ibrahimu Kabole alisema kuna uelewa mdogo pamoja na mila potofu zinazofanya jambo la hedhi kuonekana ni la aibu.
“Asilimia 40 ya wanafunzi wa kike hutoroka shule kutokana na kuzomewa,kunyanyapaliwa pamoja na kukosa mazingira rafiki wanapokuwa kwenye hedhi,” alisema Kabole.
Alisema jamii ipewe uwezo kujua jambo hilo na liongelewe kwa uwazi ili kuwajengea mazingira bora ya kusoma.
Siku ya hedhi duniani kwa mara ya kwanza imeadhimishwa nchini kwa maandamano ya wanafunzi wa kike kutokea Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi na kumalizikia viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment