Sunday, May 24, 2015

UDSM WALIA NA LUBUVA



 WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salam (UDSM), wameiomba serikali kuhakikisha inaweka mfumo madhubuti wa kuandikisha wanafunzi kwenye daftari la Kudumu la Wapiga kura ili haki yao kikatiba itekelezeke.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO), Shitindi Venance alisema, hadi sasa hakuna utaratibu wowote wa wao kuandikishwa katika daftari hilo jambo ambalo linaonyesha kuwanyima haki yao ya msingi.
“Sisi kama wanavyuo na kila aliyepo chuoni hapa ni mtu mzima ametimiza miaka 18, lakini kwa utaratibu uliopo inaonyesha dhahiri wanataka kutunyima haki yetu ya kuwachangua viongozi tunaoona wataleta mabadiliko nchini.
“Tumeamua kutoa ombi hili baada ya kuona utaratibu wa kuandikisha ukiendelea kufanyika katika majimbo yetu wakati sisi tupo chuoni tukiendelea na masomo na hadi sasa hatujapewa utaratibu wa kuandikishwa katika vyuo,” alisema Venance.
Venance alisema ni vyema serikali ikaona haja ya kufungua matawi katika vyuo mbalimbali nchini na kuandikisha wanafunzi katika daftari hilo ili wapate haki ya kumchagua kiongozi wanayemhitaji.
Alisema inasikitisha sana wao kukosa haki hiyo hadi sasa kwani vijana ndiyo wenye kuleta changamoto ya kupata viongozi wenye manufaa ambao wako tayari kuleta mageuzi ya kiuchumi katika majimbo yao.
“Tunaomba Serikali iliangalie kwa umakini suala hili kwani sisi ndiyo wenye uwezo wa kuwaelimisha wananchi vijijini kiongozi yupi anafaa hasa ukizingatia maeneo hayo baadhi yao hawana uelewa wa yupi anafaa kuwa kiongozi bora,” alisema Venance.
Alisema mzalendo wa kweli anaheshimika kwa elimu yake na si kumfundisha mtu uzalendo kwa kumpeleka jeshini ambapo aliiomba serikali kuwaelewa katika hilo

No comments:

Post a Comment