MGOMO wa wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM),
umemalizika na wanafunzi wote wameingia darasani na kuendelea na masomo kama
kawaida baada ya Bodi ya Mikopo kuwaingizia fedha zao za kujikimu walizokuwa wamecheleweshewa
kwa mujibu wa mikataba yao.
Akizungumza na FICHUA jana Waziri wa Mikopo wa Serikali ya wanafunzi wa chuo
hicho(DARUSO), Shitindi Venance alisema fedha walizokuwa wamecheleweshewa na
Bodi ya mikopo(HESLB) ziliingizwa juzi jioni hivyo kumaliza kwa mgomo huo .
Alisema wanafunzi walikuwa wakiidai Bodi hiyo jumla ya
shilingi bilioni 2.8 ambazo ni fedha za kujikimu kwa wanafunzi wanafunzi
6,120 kama inavyoainishwa kwenye
mikataba yao na Bodi hiyo.
Alisema waliingia mkataba na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu (HESLB) kuwa kila baada ya wiki nane watakuwa wanaingiziwa Sh
450,000 kwa ajili ya kujikimu mpaka mwishoni mwa wiki walikuwa hawajaingiziwa
fedha hizo na kuwasababishia maisha kuwa magumu zaidi.
Alisema Serikali iache urasimu pamoja na kufanya kazi kwa
mazoea kwa kusubiri shinikizo la migomo ndipo watekeleze majukumu yao.
“Tumekuwa tukisoma kwa shida kwa muda mrefu ambapo hata
mwaka jana tulienda kufanya mafunzo kwa vitendo(field attachment) bila kulipwa
fedha hadi tuliporejea,” alisema Venance.
Alisema Serikali inawafundisha vibaya kwani bila ya
kuiadhibu kwa migomo na mashinikizo haitekelezi jambo kitu ambacho kinajenga taswira
mbaya kwa jamii.
“Mwaka huu tunatangaza mapema kuwa kama fedha za kwenda
kwenye mafunzo kwa vitendo(field) hazitakuwepo nasi hatutaenda,” alisema
Venanc
Aidha alisema viongozi wengi walioko madarakani wanatumia
vibaya nyazifa na fedha zao kuwalaghai wanafunzi wa kike nao kwa shida
walizonazo wanajikuta wakiingia kwenye mitego hiyo.
“Tunawaona wanavyokuja na mashangingi yao kuwalaghai dada
zetu huku hawawatekelezei madai yao wawalipe kwa wakati ili wasije wakaingia
vishawishini,” alisema Venance.
Alisema anamkumbusha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kauli yake
aliyoitoa mwaka 2010 kuwa fedha za kujikimu zitakuwa zinapanda kila baada ya
miaka mitatu kwani toka kipindi hicho mpaka sasa haijawahi kupanda.
“Tangu Waziri Mkuu aliposema kuwa watakuwa wanafanya
tathmini na kupandisha fedha za kujikimu mpaka leo haijawahi kupanda japo
gharama za maisha zinapanda kila siku,” alisema
Alipotafutwa, Msemaji wa Bodi ya Mikopo, Cosmas Mwaisobwa
alisema madai ya wanafunzi wa vyuo vyote yameanza kushughulikiwa kwa kuanza na Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
No comments:
Post a Comment