TUME ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imetoa ripoti yake ya uchunguzi dhidi ya
tuhuma kwa Jeshi la Polisi za kuwapiga na kuwadhalilisha viongozi na wafuasi wa
Chama cha Wananchi (CUF), na kusema jeshi hilo lilitumia nguvu kupita kiasi na
kuwadhalilisha wanawake wawili wa chama hicho.
Akitoa
ripoti hiyo jana jijini Dar es Salaam kwa waandishi wa habari, Mwenyekiti wa
Tume hiyo, Bahame Nyanduga alisema pia jeshi hilo lilikiuka misingi ya Utawala
Bora kwa wana CUF katika tukio
lililotokea eneo la Mtoni Mtongani wakati wanachama hao wakienda kuahirisha
mkutano wao Mbagala Zakhem.
Nyanduga
alisema tukio hilo la ukiukwaji wa haki
za binadamu lilitokea Januari 27,mwaka huu ambapo taarifa zilionyesha kuwa
polisi hao waliwapiga na kuwakamata wananchi waliokuwa kwenye msafara wa
Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba.
Alisema
mambo yaliyobainika katika uchunguzi huo ni polisi kutumia nguvu kupita kiasi
na kusababisha majeraha kwa viongozi wa CUF, kuathiri baadhi ya raia maeneo ya
jirani na kukiuka misingi ya utawala bora kwa kutokuheshimu haki za binadamu.
“Tukio lile tume
yetu pia ilibaini lilikuwa na udhalilishaji dhidi ya wanawake wawili wa CUF
wakati wakikamatwa na kupelekwa mahabusu gereza la Segerea,”alisema Nyanduga.
Alisema
kutokana na uchunguzi huo na matokeo ya ripoti hiyo tume imetoa mapendekezo kwa
taasisi mbalimbali za serikali na vyama vya siasa kwa jeshi la polisi.
Alisema
miongoni mwa mapendekezo hayo ni pamoja na kuzingatia kanuni, sheria, haki za
binadamu na misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila
siku, kutoa mafunzo kwa askari wake wanaoratibu shughuli za maandamano ya raia
au vyama vya siasa.
Mengine ni
kuhakikisha askari na maafisa wake wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara yahusuyo
haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
pia katika operesheni zake lifuate
utaratibu na kanuni za jeshi kwa kuzingatia jinsia za watumiwa na askari wanao
washughulikia.
Wakati
huohuo, Tume imetoa angalizo kwa polisi kuzingatia uhuru wa vyombo vya habari
wakati wa utekelezaji wa operesheni zake na jeshi la Magereza lisitishe mara
moja kufanya upekuzi wa watuhumiwa na kuepuka udhalilishaji wa heshima na utu
wa binadamu.
Pia tume
hiyo imekitaka chama cha CUF kutafuta namna ya kuboresha mahusiano na polisi
ili kuepuka mivutano isiyo na tija katika shughuli za kisiasa, kuepusha vurugu
na kulinda haki za binadamu.
“CUF ilikiri kumiliki kikundi cha ulinzi cha Blue
Guard hivyo tunakiomba kuzingatia katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977 inayozuia chama cha siasa kuwa na
kikundi cha mtazamo wa aina hiyo.
No comments:
Post a Comment